Trump akataa mjadala wa pili wa TV akisema 'umechelewa sana'
Trump akataa mjadala wa pili wa TV akisema 'umechelewa sana'

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump amesema hatashiriki katika mjadala wa pili wa televisheni kabla ya uchaguzi wa urais mwezi Novemba.
Wakati Makamu wa Rais Kamala Harris, mgombea wa Chama cha Democratic , alikubali mwaliko wa mdahalo wa CNN tarehe 23 Oktoba, mgombea mteule wa Republican Trump aliambia mkutano kuwa "umechelewa" kwani upigaji kura tayari umeanza.
Timu ya kampeni ya Harris ilisema kwamba kutokana na rais huyo wa zamani kudai kuwa alishinda mjadala wao wa awali huko Philadelphia mapema mwezi huu anapaswa kukubali.
Kura za maoni zilizopigwa baada ya mkutano huo zilipendekeza kuwa wengi wa watazamaji waliamini kuwa makamu wa rais alimshinda mpinzani wake.
Baada ya mjadala wa Septemba 10, Trump alisema hakutakuwa na mijadala zaidi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara huko Wilmington, North Carolina siku ya Jumamosi, alidai ushindi katika mdahalo huo wa awali na kusema "umechelewa sana" kwa mwingine.
"Upigaji kura tayari umeanza," alisema, akimshutumu Harris kwa kutafuta duru nyingine yapambano "kwa sababu anapoteza vibaya."
Katika taarifa siku ya Jumamosi, mwenyekiti wa kambi ya kampeni ya Harris-Walz Jen O'Malley Dillon alisema kuwa Wamarekani "wanastahili fursa nyingine" ya kuona mjadala wa Harris na Trump kabla ya uchaguzi wa Novemba.
"Itakuwa jambo lisilokuwa la kawaida katika historia ya kisasa kwa kuwa na mjadala mmoja tu wa uchaguzi mkuu," alisema. "Mijadala inatoa fursa ya kipekee kwa wapiga kura kuona wagombea bega kwa bega na kutathmini maono yao ya ushindani kwa Marekani."
Kwenye X, ambayo zamani ilikuwa Twitter, Harris alisema "amekubali mwaliko wa mjadala" kwa furaha na anatumai Trump pia atashiriki.
Comments
Post a Comment